Friday 19 October 2012

IKULU IMESEMA HIVI KUHUSIANA NA DK ULIMBOKA

SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dkt. Stephen Ulimboka, kusisitiza kwamba alitekwa na mtu anayefanya kazi Ikulu, Ramadhan Ighondu, Ikulu imehamanika na kujitetea kwamba madai hayo ni ya kipuuzi.

         *Tafadhali bofya hapa kurejea kuisoma nakala ya taarifa kamili aliyoitoa Dkt. Ulimboka.

Jana Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alisisitiza: “Ikulu iliishajibu. Tulisema haihusiki, na Rais Jakaya Kikwete amepata kuzungumza juu ya jambo hili mara nyingi.”

Rweyemamu, bila ya kufafanua zaidi alisema, “Naomba uninukuu; haya madai ni upuuzi… hiki kitu kilishajibiwa.”

Alipoulizwa kama anamfahamu Ramadhan Ighondu, Rweyemamu akisisitiza kuwa Ikulu haihusiki naye.

Mwandishi akamwuliza Rweyemamu ni hatua gani ambazo Ikulu itamchukulia Ighondu kama mfanyakazi wao.

Swali hilo lilionekana kumkera Rweyemamu aliyejibu kwa ukali, “Kama Ikulu haihusiki, hatuna cha kufanya juu ya jambo hilo; mnakaa mnalea maneno ya kipuuzi… Ikulu imwajibishe kuhusu nini? Haihusiki!”

Alipobanwa zaidi alisema kama kuna watu wanasema hivyo waende wakaripoti polisi.

Kauli ya jana ya Rweyemamu ni ya pili kutolewa na Ikulu kuhusu Dkt. Ulimboka. Mara ya kwanza, ilipotolewa na Rais Jakaya Kikwete alipokutana na baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, akasema, “Dk. Ulimboka ana nini mpaka Ikulu imteke? Tumteke ili iweje?”

Kikwete alikwenda mbali zaidi na kusema hata Dk. Ulimboka mwenyewe alipokwenda Ikulu akiwa na viongozi wenzake alinyamaza kimya tu na kwamba waliokuwa wakizungumza ni wengine.

Hata hivyo, kwa kuwa Ikulu imesema haihusiki, na Dk. Ulimboka mwenyewe ametamka kwamba anamjua aliyemtesa, na kwamba anafanya kazi Ikulu, ni juu ya umma kuamua nani anasema ukweli.

Wakati Ikulu ikisema hayo, Jeshi la Polisi ambalo lilimtia mbaroni raia wa Kenya na kumpeleka mahakamani kujibu tuhuma za kumteka na kumtesa daktari huyo, nalo limesita kubainisha kama litamkamata na kumhoji Ighondu, ambaye ametajwa rasmi na shahidi wa kwanza halisi katika suala hili, Dkt. Ulimboka.

Maofisa wa jeshi hilo wametupiana mpira kila mmoja akidai hahusiki na suala hilo.

Kwa upande wa polisi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alijitetea akisema suala hilo liko kwa mkubwa wake wa kazi, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Maanumba, na kwamba atafutwe kwa ajili ya kulitolea ufafanuzi, “Gazeti lenu juzi nililisifia sana nikalitolea mfano mzuri; watu hawawezi kutuchezea tu na kutishia mamlaka iliyopo kama hakuna sheria. Lazima kila mmoja afuate sheria. Hilo suala liko kwa DCI na sisi polisi tuna nidhamu ya kazi. Suala likiwa kwa mkubwa wako huwezi kulizungumzia. Tambua faili lipo kwao na mimi sina uwezo wa kulizungumzia,” alisema.

Alipobanwa zaidi kuwa Dkt. Ulimboka ameshamtaja aliyemtesa na kwamba yuko tayari kuwapa ushirikiano na kutoa ushahidi mbele ya tume huru, Kova alisema, “Hivi wewe unanitafuta nini? Nimekwambia sina uwezo nalo; au hutaki ushirikiano na mimi? Hilo swali lako ni sawa na kumuuliza kipofu pale unapaonaje!?”

Naye DCI Manumba alipopigiwa simu, alijibu kwa kifupi akisema aulizwe msemaji wa jeshi hilo. Akakata simu.

Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, alipoulizwa alisema suala hilo liko kwenye uchunguzi, hivyo hawezi kulitolea ufafanuzi. Senso alipobanwa zaidi, alisisitiza, “Tafadhali, sina maelezo zaidi ya hayo. Kukiwa na kitu kipya tutaandaa.”

Sunday 7 October 2012

HAPPYBIRTHDAY PRESIDENT KIKWETE

Leo tarehe 7-10 ni siku ya kuzaliwa ya mheshimiwa rais wetu wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania ,Jakaya Mrisho Kikwete.Mungu akujalie busara nyingi na moyo wa kuliendeleza Taifa hili.

Friday 5 October 2012

KESI YA LULU YARUDI KISUTU KWAAJILI YA KUANZA UPYA

KESI ya mauaji inayomkabili msanii wa filamu za maigizo nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’ anayedaiwa kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba ‘The Great’ ambayo leo ilitakiwa kutolewa maamuzi ya umri na Mahakama ya Rufaa imerudishwa mahakama ya Kisutu kuanza upya.

Akitoa maamuzi hayo, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo yenye maamuzi ya mwisho hapa nchini, Zahra Marume amesema utaratibu uliotumika kuifikisha kesi hiyo mahakamani hapo ulikuwa na makosa hivyo kuamuru kesi hiyo kurudi mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam.




TANZANIA YAPOKEA MSAADA WA BILIONI 352 KUTOKA KWA WAJERUMANI

Ujerumani imetoa jumla ya shilingi bilioni 352( euro milioni 176) kwa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika kipindi miaka mitatu ijayo.
Makubaliano ya msaada huo yamesaini jana jijini na Waziri wa Fedha Dr. William Mgimwa kwa upande wa Tanzania na Balozi wa Ujerumani nchini Kluas Peter Brandes.
Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo kwa niaba ya Tanzania Waziri wa Fedha dr. Mgimwa alisema kuwa fedha hizo zitasaidia shughuli mbali za maendeleo katika kipindi cha mwaka 2012/13- hadi 2014/15.
Alisema kuwa msaada huo unalenga maeneo ya kuboresha utawala bora katika serikali za mitaa, kusaidia sekta ya afya , nishati , maliasili, maji, na kuboresha programu ya usimamizi wa fedha za umma.
Dr. Mgimwa aliongeza kuwa eneo jingine ambapo hizo zitaelekezwa ni pamoja na kusaidia mfuko wa bajeti kwa kipindi miaka mitatu hiyo na kusaidia ofisi ya Taifa ya Mkaguzi wa hesabu za serikali .
Alisema kuwa miradi hiyo itasaidia kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) na hivyo kuboresha hali ya uchumi na kijamii ya wananchi.
Aidha Waziri huyo wa Fedha alimuhakikisha Balozi wa Ujerumani nchini kuwa , Serikali itahakikisha fedha za msaada zinatuma katika maeneo yalipangwa kwa manufaa ya wananchi ili matokeo yake yaweze kuonyesha thamani ya fedha waliyotoa.
Naye Balozi Brandes alisema kuwa Nchi yake itaendelea kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu na Tanzania ili kufikia malengo ya kupambana na umaskini na hivyo kuboresha maisha ya Watanzania hasa waishio vijijini.
Aliongeza kuwa msaada waliotoa utasaidia wakazi wa mijini kupata maji safi na salama kwa ajili ya kujikinga na magonjwa yatokanayo na maji yasiyo salama.

WEZI WA UMEME WABABWA


 
WATU watano wamekamatwa kwa makosa ya wizi wa umeme, wakitumia  njia za kuharibu mita na kujiunganishia huduma hiyo bila ya kufuata taratibu za Shirika la Umeme nchini (Tanesco). 
Msimamizi wa operesheni ya ukaguzi wa mita uliyofanyika Temeke, Dar es Salaam  juzi,  Johari Nasibu, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa jumla ya nyumba 80 zilifanyiwa ukaguzi na baadhi ya hizo kukutwa na makosa hayo.
Alisema  miongoni mwa makosa waliyotwa nayo wateja hao watano ni pamoja na wizi kujiunginishia umeme nje ya mita na kuchezea mita kwa kuziharibu ili ziweze kuandika matumitumizi stahiki.
“Kama tunavyofanya siku zote kwenye kazi  hii leo hii tumefanya hapa Mtoni eneo la Relini, tumefanikiwa kukuta mita nane zikiwa na makosa mbalimbali na hatua za haraka tulizo zichukua ni kuwasitishia huduma  kwanza kabla ya kufanya tathmini ya hasara tuliyopata ili waweze kutulipa na kama hawajalipa tunawafikisha mahakamani” alisema Nasibu.
 Johari alisema kiasi kikubwa cha umeme kimekuwa kikiibiwa na baadhi ya watu ambao siyo waaminifu huku  shirika hilo likiingia hasara bila kutarajia.
Aidha, shirika hilo linatarajia kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote iwapo watabainika mojamoja kwa moja na kujihusisha vitendo vya kulihujumu shirika hilo.
Akifafanua kuhusu  utaalamu unaotumika ili kukotoa na  kugundua kiwango cha umeme kinachoibwa  na wateja wasiokuwa waminifu  Mmoja wa wakaguzi kwenye operesheni hiyo, Omari Mgasa, alisema kazi hiyo nirahisi kutokana na kuorodhesha idadi ya vifaa vyote vinavyotumia nishati hiyo katika nyumba pamoja na kuangalia kiwango cha matumizi ya mteja katika kipindi chote tangu alipounganishiwa huduma hiyo.
Pamoja na mafanikio ya operesheni  hiyo ya ukaguzi wa mita, alisema bado opersheni hiyo inakabiliwa na  changamoto mbalimbali, moja wapo ikiwa nikukosekana ushirikiano wakutosha  kwa  baadhi ya wateja ambao kwa makusudi wamekuwa wakifunga nyumba zao na kukimbia pindi wawaonapo wafanyakazi wa shirika hilo hasa wanapoandamana na askari polisi.
Katika hatua nyingine, Mgasa alisema kuna baadhi ya  maeneo ambayo wateja wanaotuhumiwa kufanya vitendo vya hujuma kwa kuiba umeme, shirika limepokea taarifa hizo ambapo limefika katika maeneo hayo na kusitisha huduma kwa wateja hao ikiwa ni pamoja kuwakatia nya kwenye nguzo kwa ajili ya hatua nyingine.

MATOKEO YA CHAGUZI ZA CCM-NEC

CHAGUZI ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimeendelea katika maeneo mbalimbali nchini ambapo sura mpya zimezidi kutikisa na kuwabwaga makada wa muda mrefu.

Tanga Mjini

Mbunge wa Tanga Mjini, Bw. Omari Nundu, ameanguka vibaya katika kinyang’anyiro cha kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), baada ya kupata kura 127 kati ya kura 1,183 zilizopigwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu.

Uchaguzi huo ulikuwa na mchuano mkali kati ya Bw. Nundu na aliyekuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Bw. Salim Kisauji aliyeibuka ushindi baada ya kupata kura 556.

Kushindwa vibaya kwa Bw. Nundu ambaye alikuwa Waziri wa Uchukuzi, kunamuweka njia panda katika medani ya siasa. Baadhi ya wana CCM mjini hapa walidai kushindwa kwa Bw. Nundu ni ishara mbaya kwake kuweza kutetea kiti chake cha ubunge kwa tiketi ya CCM kwani idadi ndogo ya kura alizopata ni ishara kuwa hana nafasi tena katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Akitangaza matokeo hayo jana alfajiri, Msimamizi wa uchaguzi huo Bw. Acheny Maulid, alimtangaza Bw. Kisauji kuwa mshindi wa nafasi ya ujumbe wa NEC. Alisema kura zilizopigwa zilikuwa 1,183 wakati nane ziliharibika na kura 1,175 zilikuwa halali. Katika uchaguzi huo Bi. Saumu Bendera alipata kura 458 na Bw. Salehe Masoud akipata 34.

Katika nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tanga, kiti hicho kilichukuliwa na Bw. Kassim Mbuguni aliyepata kura 662,  akifuatiwa na Bi. Mwanshamba Pashua (354) ambapo Bw. Samwel Kamote ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya mbalimbali nchini alipata kura 200 na Bw. Salim Mazrui akipata 98. Kura zilizopigwa zilikuwa 1,034 zilizoharibika 18, ambapo kura halali zilikuwa 1,016.

Akizungumza baada ya kuthibitishwa kuwa mjumbe wa NEC, Bw. Kisauji, aliahidi kuendeleza mshikamano ili kuongoza harakati za kukiimarisha chama hicho, “Nitaongeza kasi ya kuisimamia kikamilifu Serikali Wilaya ya Tanga ambapo siku za karibuni, kulikuwepo na udhaifu mkubwa uliochangia kuleta malalamiko dhidi ya Serikali,” alisema na kuwa, aliyekuwa mpinzani wake Bi. Bendera ataendelea kushirikiana nae kuhakisha wanasimamia wote utekelezaji wa ilani ya chama hicho na kuzikomboa kata tisa zilizoko upinzani kutoka CUF ili zirejeshwe CCM.

Hata hivyo, aliyekuwa Mwenyekiti wa muda katika uchaguzi huo Bw. Athuman Makalo, aliwataka wagombea wote waende mbele kuelezea mazingira ya uchaguzi huo.

Baadhi ya wagombea walioshindwa waliondoka ukumbini ambapo Bi. Mwanshamba Pashua, ambaye alishika nafasi ya pili katika nafasi ya Uenyekiti wa CCM Wilaya, ndiye aliyekwenda kuwashukuru wapiga kura.

Bunda

Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, Wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, wapo katika ushindani mkali kila mmoja akihaha kusaka kura kwa wajumbe.

Katika uchaguzi uliofanyika jana, mgombea wa nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha, Bw. John Kitang’osa, ambaye ni Katibu wa mbunge wa Bunda, Bw. Stephen Wassira, alibwagwa na kijana Bw. Mukwabe Sila.

Mgombea mwingine katika nafasi hiyo alikuwa Bw. Sarate Mimi ambaye ni mmoja kati ya Maofisa Wakaguzi wa Ndani katika Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Nafasi ya Katibu Uenezi Wilaya ilichukuliwa na Bw. Janes Sariro, ambaye aliwabwaga Bw. Kondoro Bega na Bw. Juma Sanga.

Bw. Christopher Sanya, Bw. Makongoro Nyerere na Bw. Enock Chambili, ambao wanagombea nafasi ya Uenyekiti Mkoa, waliomba kura kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilayani humo ambapo uchaguzi huo utafanyika Oktoba 13 mwaka huu.

Akiomba kura kwa wajumbe hao, Bw. Sanya alisema vigogo ndani ya CCM ndio wanaoendekeza makundi hivyo ni vyema wanachama waingize sura mpya ili kuleta umoja ndani ya chama hicho, “Wanaodai kumaliza makundi ndani ya CCM wanasema kwa mdomo tu, lakini haitoki moyoni kwa sababu wameshika madaraka hayo siku nyingi, dawa ya kumaliza makundi ni kuwachagua makada wasioegemea upande wowote,” alisema Bw. Sanya na kuongeza: “Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, utakuwa mgumu kwa chama chetu kama viongozi ambao watachaguliwa wataendeleza siasa za makundi.”

Naye Bw. Makongoro Nyerere, alidai mwaka 2007 aliipokea CCM iliyosambaratika mkoani humo iliyojaa siasa ya chuki na makundi ambapo kazi aliyoifanya ni kurejesha umoja katika chama hicho. Alisema viongozi wa kitaifa ndio wanaosambaza tofauti zao hadi kwenye matawi ya chama na kusambaratisha wanachama.

Bw. Chambili alidai yeye ni kiongozi asiyeogopa upinzani na yuko tayari kuhakikisha hakuna jimbo ambalo litachukuliwa na upinzani mkoani humo kama watamchagua katika nafasi hiyo.

Hata hivyo baadhi ya wajumbe na makada wa CCM, walidai wagombea wote wa nafasi, wamekiuka agizo la Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, “Hivi karibuni akiwa mjini Dodoma kwenye kikao cha NEC, baada ya kupitishwa majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali, Rais Kikwete aliwahadharisha wagombea wa nafasi zote kutowafuata wapiga kura ili kuomba huruma yao kabla ya siku ya uchaguzi,” walisema wajumbe hao.

Same
Mkuu wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Bw. Clement Kapufi, aliibuka na ushindi katika nafasi ya wajumbe watano ambao wataiwakilisha Wilaya hiyo katika Mkutano Mkuu Taifa.

Wengine walioshinda katika nafasi hiyo ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bw. Christopher Irira, Ummy Mkumbwa, Bi. Veronica Mmbaga na Zabihuna Irigo.

Katika uchaguzi huo, Mwenyekiti wa CCM wilayani humo Bw. Augustine Kessy, alitetea nafasi yake baada ya kupata kura 855 dhidi ya Bw. Yahya Mnzava (324) na Azza Nisaghurwe (153).

Bw. Ali Mmbaga alishinda katika nafasi ya ujumbe wa NEC wilayani humo baada ya kupata kura 832, wakati Bw. Joseph
Kateri (438), ambapo Bw. Joseph Mnzava, alipita bila kupingwa kwenye nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha.

Mwanga

Mwenyekiti wa CCM aliyemaliza muda wake Bw. Urban Masewa, alitetea nafasi hiyo baada ya kupata kura 527 ambapo mpinzani wake Bw. Suleiman Mruttu aliepata kura 252.

Wakili wa kujitegemea Bw. Joseph Tadayo, alishinda ujumbe wa NEC wilayani humo baada ya kuzoa kura 535 dhidi ya Bw. Kuria Msuya, (255) na Kanali mstaafu Saidi Msuya (18).

Bw. Suleiman Mfinanga, alimrithi Waziri Mkuu mstaafu, Bw. Cleopa Msuya katika nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha,
baada ya kupita bila kupingwa.

Rombo
Bw. Wilbard Ringia alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM wilayani humo kwa kura 398 wakati Bw. Rogatus Matoli (300), ambapo Bw. Evod Mmmanda, alishinda ujumbe wa NEC wilayani humo kwa kura 380, Bw. Calisti Shirima (311) na Bw. Sabas Asenga aliepata kura 15. 

---
Taarifa hii ni kwa mujibu wa Waandishi wa habari Raphael Okello, Heckton Chuwa na Benedict Kaguo wa gazeti la Majira


Thursday 20 September 2012

DO YOU KNOW THIS?


A MAN PANNISH HIS WIFE


SIJAUZA ENEO LA KIGAMBONI; JAKAYA KIKWETE


Rais Kikwete akiweka jiwe la msingi kuashiria kuzindua rasmi ujenzi wa Daraja la Kigamboni katika hafla iliyofanyika huko Kurasini jijini Dar es Salaam leo mchana. Kushoto ni Waziri wa Ujenzi Dkt. Magufuli na wa pili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Dkt. Ramadhani Dau. NSSF itagharamia asilimia 60 za ujenzi wa daraja hilo na Serikali asilimia 40. (Picha: Freddy Maro/IKULU)

 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Alhamisi, Septemba 20, 2012, ameweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Daraja la Kigamboni, Dar es Salaam kwa kuwaonya watu ambao amewaeleza kuwa wanavyo viwanda vya kutunga uongo kuacha tabia hiyo na kuelekeza nguvu kwenye maendeleo.

Aidha, Rais Kikwete amewahakikishia wakazi wote wa Kigamboni ambao wanaondolewa katika maeneo yao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa daraja hilo na ujenzi wa Mji Mpya wa Kigamboni kuwa watalipwa stahili na haki zao zote.

Daraja hilo la Kigamboni ambalo wazo la kujengwa kwake lilibuniwa kwa mara ya kwanza zaidi ya miaka 30, tokea mwaka 1978, wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, linajengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 214.6 na litakuwa tayari katika muda wa miezi 36 ijayo, ingawa muda huo unaweza kupungua na kubakia miezi 30.

Daraja hilo ambalo litakuwa na urefu wa mita 680 linagharimiwa kwa pamoja na Serikali na Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF ambalo litachangia kiasi cha asilimia 60 na Serikali asilimia 40.

Daraja hilo ambalo litakuwa na jumla ya barabara za kupitisha magari sita kwa wakati mmoja linajengwa na makampuni mawili ya China ambayo ni China Railway Construction Engineering Group na China Railway Major Bridge Engineering Company na mhandisi msimamizi wa ujenzi huo ni Kampuni ya Misri.

Daraja hilo litapunguza adha ya usafiri kati ya Kigamboni na Dar es Salaam ambao kwa sasa unategemea vivuko, ama boti ndogo, mitumbwi ama wenye magari kulazimika kufanya mzungumo wa kilomita 52. Kwa uamuzi wa sasa, wavuka kwa miguu ambao watakuwa na njia maalum kwenye daraja hilo pamoja na waendesha baiskeli watavuka bure bila malipo yoyote.

Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali haiwezi kudhulumu wananchi wake na hivyo watu wote ambao wanastahili fidia kutokana na ujenzi wa daraja hilo na mji mpya wa Kigamboni watalipwa haki na stahiki zao.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake haitaruhusu mtu yoyote kuzuia ama kuchelewesha miradi ya maendeleo ambayo inalenga kunufaisha watu wengi.

Rais Kikwete pia amewaonya watu ambao wamelifanya suala la kutunga na kusema uongo kama sehemu ya utamaduni wao. “Watu wana viwanda vya kuzalisha uongo. Wanashinda wanasambaza uongo kwenye mitandao, kila mahali. Wamepata hata kusema kuwa mimi nimemuuzia George Bush eneo la Kigamboni. Bush aje kufanya nini Kigamboni?”

Rais pia amesema kuwa wapo watu ambao hawapendi maendeleo ya nchi. “Wanatamani kila siku tushindwe kuwaletea wananchi maendeleo. Lakini watakufa kwa kihoro kwa sababu hatutashindwa. Kila tulilosema tutalifanya, litafanyika”.

Amesema kuwa thamani kubwa ya vyama vya siasa ni maendeleo ya wananchi. “Lakini wapo wenzetu ambao wanaudhika wakiona maendeleo. Wanapenda hata daraja hili lisijengwe. Leo hawatalala usingizi. Kazi ya vyama vya siasa ni kuweka maslahi yetu sote mbele.”

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
20 Septemba, 2012

WAISLAMU KUKUSANYIKA JANGWANI KUPINGA FILAMU YA INNOCENCE OF MUSLIM

Amiri wa Shura ya maimamu Tanzania, Shekh Mussa Kundecha (kulia) akiwa masheikh wa Taasisi ya Umoja wa Wanazuoni wa Kiisilam  wakati wa kutangaza hatua ambazo waislamu watazichukua ili kupinga  Filamu iliyotengenezwa nchini Marekani ya kumkashifu Mtume Mohamad (SAW).Alitangaza
Msimamo uliotangazwa na waislamu hao katika mkutano huo  ni wakufanyika mkutano mkubwa  kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam ambapo waisilamu wote watakusanyika hapo kulaani Filamu hiyo.

Hawa ni waislamu waliohudhuria mkutano huo kwenye msikiti wa Kichangani jijini Dar es Salaam wakati wa Sala ya Ala -asiri leo, wakifuatilia kwa makini matamko na mawaidha ya masheikh mbalimbali

Friday 14 September 2012

SERIKALI IIGE MFANO HUU


Shamba la kilimo cha umwagiliaji cha Mbogamboga la Ngongoseke lililoko katika kijiji cha Nsola wilayani Magu ni mfano wa kuigwa katika matumizi ya ziwa Victoria. Pichani, nyanya ndogondogo maarufu kwa jina la nyanyapori zikiwa zimelimwa kitalaam kwenye shamba hilo ambalo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alilitembelea Septemba 13, 2012. (Picha: Ofisi ya Waziri Mkuu)


SERIKALI YATONYWA

Programme Manager kutoka Zambia Bw, Bou Muchaba Iwa akisikiliza kwa makini katika mkutano huo

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Muungano wa Mashirika yasiyo ya kiserikali (TANGO) akizungumza na wadau mbalimbali lambapo ameishauri serikali kuongeza  uwekezaji    katika huduma za jamii  nchini kuliko kuwekeza zaidi kwenye uchumi.Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Muungano wa mashirika yasiyo ya serikali (TANGO),Bw.Ngunga Tepani katika mkutano wa wadau wa kupinga umasikini (SADC Regional Poverty Observatory) yaliyofanyika katika Hoteli Ya Blue Pearl.


Thursday 13 September 2012

KIONGOZI WA FREEMASON KUMWAGIKA LEO CLOUDS TV

Anndy Chande; Gerald Hando aliyeshika kikombe cha chai (kikombe mkononi)
Kinara wa kundi la Freemasons katika eneo la Afrika Mashariki, Jayantilal Keshavji Chande maarufu kama Sir Andy Chande, leo  kuanzia saa 3:00 usiku ataanika mambo mengi kuhusiana na undani wa kundi hilo wakati atakapozungumza na mtangazaji Gerrard Hando wa kituo cha televisheni cha Clouds "The Peoples Station".

Akizungumza kupitia kipindi cha Power Breakfast cha redio ya Clouds FM leo asubuhi, mtangazaji Hando ambaye ndiye aliyefanya mahojiano na Sir Chande, amesema kuwa mambo mengi kuhusu undani wa Freemasons na namna wanavyofanya kazi zao, yameelezewa kwa kina na kigogo huyo wa zamani wa kundi hilo duniani.

Amesema kuwa mahojiano hayo yatarushwa kuanzia leo kupitia kipindi chao kipya kiitwacho "The Interview', ambacho kitarushwa kuanzia leo usiku.

Namna ya kujiunga na Freemasons na mahala liliko hekalu la kundi hilo jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kuzungumziwa na Sir Chande.

Kigogo huyo wa Freemasons amekuwa karibu sana na viongozi wa juu serikalini, wakiwamo marais wastaafu wote wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin William Mkapa na sasa, Rais Jakaya Kikwete.