Friday 19 October 2012

IKULU IMESEMA HIVI KUHUSIANA NA DK ULIMBOKA

SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dkt. Stephen Ulimboka, kusisitiza kwamba alitekwa na mtu anayefanya kazi Ikulu, Ramadhan Ighondu, Ikulu imehamanika na kujitetea kwamba madai hayo ni ya kipuuzi.

         *Tafadhali bofya hapa kurejea kuisoma nakala ya taarifa kamili aliyoitoa Dkt. Ulimboka.

Jana Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alisisitiza: “Ikulu iliishajibu. Tulisema haihusiki, na Rais Jakaya Kikwete amepata kuzungumza juu ya jambo hili mara nyingi.”

Rweyemamu, bila ya kufafanua zaidi alisema, “Naomba uninukuu; haya madai ni upuuzi… hiki kitu kilishajibiwa.”

Alipoulizwa kama anamfahamu Ramadhan Ighondu, Rweyemamu akisisitiza kuwa Ikulu haihusiki naye.

Mwandishi akamwuliza Rweyemamu ni hatua gani ambazo Ikulu itamchukulia Ighondu kama mfanyakazi wao.

Swali hilo lilionekana kumkera Rweyemamu aliyejibu kwa ukali, “Kama Ikulu haihusiki, hatuna cha kufanya juu ya jambo hilo; mnakaa mnalea maneno ya kipuuzi… Ikulu imwajibishe kuhusu nini? Haihusiki!”

Alipobanwa zaidi alisema kama kuna watu wanasema hivyo waende wakaripoti polisi.

Kauli ya jana ya Rweyemamu ni ya pili kutolewa na Ikulu kuhusu Dkt. Ulimboka. Mara ya kwanza, ilipotolewa na Rais Jakaya Kikwete alipokutana na baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, akasema, “Dk. Ulimboka ana nini mpaka Ikulu imteke? Tumteke ili iweje?”

Kikwete alikwenda mbali zaidi na kusema hata Dk. Ulimboka mwenyewe alipokwenda Ikulu akiwa na viongozi wenzake alinyamaza kimya tu na kwamba waliokuwa wakizungumza ni wengine.

Hata hivyo, kwa kuwa Ikulu imesema haihusiki, na Dk. Ulimboka mwenyewe ametamka kwamba anamjua aliyemtesa, na kwamba anafanya kazi Ikulu, ni juu ya umma kuamua nani anasema ukweli.

Wakati Ikulu ikisema hayo, Jeshi la Polisi ambalo lilimtia mbaroni raia wa Kenya na kumpeleka mahakamani kujibu tuhuma za kumteka na kumtesa daktari huyo, nalo limesita kubainisha kama litamkamata na kumhoji Ighondu, ambaye ametajwa rasmi na shahidi wa kwanza halisi katika suala hili, Dkt. Ulimboka.

Maofisa wa jeshi hilo wametupiana mpira kila mmoja akidai hahusiki na suala hilo.

Kwa upande wa polisi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alijitetea akisema suala hilo liko kwa mkubwa wake wa kazi, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Maanumba, na kwamba atafutwe kwa ajili ya kulitolea ufafanuzi, “Gazeti lenu juzi nililisifia sana nikalitolea mfano mzuri; watu hawawezi kutuchezea tu na kutishia mamlaka iliyopo kama hakuna sheria. Lazima kila mmoja afuate sheria. Hilo suala liko kwa DCI na sisi polisi tuna nidhamu ya kazi. Suala likiwa kwa mkubwa wako huwezi kulizungumzia. Tambua faili lipo kwao na mimi sina uwezo wa kulizungumzia,” alisema.

Alipobanwa zaidi kuwa Dkt. Ulimboka ameshamtaja aliyemtesa na kwamba yuko tayari kuwapa ushirikiano na kutoa ushahidi mbele ya tume huru, Kova alisema, “Hivi wewe unanitafuta nini? Nimekwambia sina uwezo nalo; au hutaki ushirikiano na mimi? Hilo swali lako ni sawa na kumuuliza kipofu pale unapaonaje!?”

Naye DCI Manumba alipopigiwa simu, alijibu kwa kifupi akisema aulizwe msemaji wa jeshi hilo. Akakata simu.

Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, alipoulizwa alisema suala hilo liko kwenye uchunguzi, hivyo hawezi kulitolea ufafanuzi. Senso alipobanwa zaidi, alisisitiza, “Tafadhali, sina maelezo zaidi ya hayo. Kukiwa na kitu kipya tutaandaa.”

Sunday 7 October 2012

HAPPYBIRTHDAY PRESIDENT KIKWETE

Leo tarehe 7-10 ni siku ya kuzaliwa ya mheshimiwa rais wetu wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania ,Jakaya Mrisho Kikwete.Mungu akujalie busara nyingi na moyo wa kuliendeleza Taifa hili.

Friday 5 October 2012

KESI YA LULU YARUDI KISUTU KWAAJILI YA KUANZA UPYA

KESI ya mauaji inayomkabili msanii wa filamu za maigizo nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’ anayedaiwa kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba ‘The Great’ ambayo leo ilitakiwa kutolewa maamuzi ya umri na Mahakama ya Rufaa imerudishwa mahakama ya Kisutu kuanza upya.

Akitoa maamuzi hayo, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo yenye maamuzi ya mwisho hapa nchini, Zahra Marume amesema utaratibu uliotumika kuifikisha kesi hiyo mahakamani hapo ulikuwa na makosa hivyo kuamuru kesi hiyo kurudi mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam.




TANZANIA YAPOKEA MSAADA WA BILIONI 352 KUTOKA KWA WAJERUMANI

Ujerumani imetoa jumla ya shilingi bilioni 352( euro milioni 176) kwa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika kipindi miaka mitatu ijayo.
Makubaliano ya msaada huo yamesaini jana jijini na Waziri wa Fedha Dr. William Mgimwa kwa upande wa Tanzania na Balozi wa Ujerumani nchini Kluas Peter Brandes.
Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo kwa niaba ya Tanzania Waziri wa Fedha dr. Mgimwa alisema kuwa fedha hizo zitasaidia shughuli mbali za maendeleo katika kipindi cha mwaka 2012/13- hadi 2014/15.
Alisema kuwa msaada huo unalenga maeneo ya kuboresha utawala bora katika serikali za mitaa, kusaidia sekta ya afya , nishati , maliasili, maji, na kuboresha programu ya usimamizi wa fedha za umma.
Dr. Mgimwa aliongeza kuwa eneo jingine ambapo hizo zitaelekezwa ni pamoja na kusaidia mfuko wa bajeti kwa kipindi miaka mitatu hiyo na kusaidia ofisi ya Taifa ya Mkaguzi wa hesabu za serikali .
Alisema kuwa miradi hiyo itasaidia kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) na hivyo kuboresha hali ya uchumi na kijamii ya wananchi.
Aidha Waziri huyo wa Fedha alimuhakikisha Balozi wa Ujerumani nchini kuwa , Serikali itahakikisha fedha za msaada zinatuma katika maeneo yalipangwa kwa manufaa ya wananchi ili matokeo yake yaweze kuonyesha thamani ya fedha waliyotoa.
Naye Balozi Brandes alisema kuwa Nchi yake itaendelea kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu na Tanzania ili kufikia malengo ya kupambana na umaskini na hivyo kuboresha maisha ya Watanzania hasa waishio vijijini.
Aliongeza kuwa msaada waliotoa utasaidia wakazi wa mijini kupata maji safi na salama kwa ajili ya kujikinga na magonjwa yatokanayo na maji yasiyo salama.

WEZI WA UMEME WABABWA


 
WATU watano wamekamatwa kwa makosa ya wizi wa umeme, wakitumia  njia za kuharibu mita na kujiunganishia huduma hiyo bila ya kufuata taratibu za Shirika la Umeme nchini (Tanesco). 
Msimamizi wa operesheni ya ukaguzi wa mita uliyofanyika Temeke, Dar es Salaam  juzi,  Johari Nasibu, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa jumla ya nyumba 80 zilifanyiwa ukaguzi na baadhi ya hizo kukutwa na makosa hayo.
Alisema  miongoni mwa makosa waliyotwa nayo wateja hao watano ni pamoja na wizi kujiunginishia umeme nje ya mita na kuchezea mita kwa kuziharibu ili ziweze kuandika matumitumizi stahiki.
“Kama tunavyofanya siku zote kwenye kazi  hii leo hii tumefanya hapa Mtoni eneo la Relini, tumefanikiwa kukuta mita nane zikiwa na makosa mbalimbali na hatua za haraka tulizo zichukua ni kuwasitishia huduma  kwanza kabla ya kufanya tathmini ya hasara tuliyopata ili waweze kutulipa na kama hawajalipa tunawafikisha mahakamani” alisema Nasibu.
 Johari alisema kiasi kikubwa cha umeme kimekuwa kikiibiwa na baadhi ya watu ambao siyo waaminifu huku  shirika hilo likiingia hasara bila kutarajia.
Aidha, shirika hilo linatarajia kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale wote iwapo watabainika mojamoja kwa moja na kujihusisha vitendo vya kulihujumu shirika hilo.
Akifafanua kuhusu  utaalamu unaotumika ili kukotoa na  kugundua kiwango cha umeme kinachoibwa  na wateja wasiokuwa waminifu  Mmoja wa wakaguzi kwenye operesheni hiyo, Omari Mgasa, alisema kazi hiyo nirahisi kutokana na kuorodhesha idadi ya vifaa vyote vinavyotumia nishati hiyo katika nyumba pamoja na kuangalia kiwango cha matumizi ya mteja katika kipindi chote tangu alipounganishiwa huduma hiyo.
Pamoja na mafanikio ya operesheni  hiyo ya ukaguzi wa mita, alisema bado opersheni hiyo inakabiliwa na  changamoto mbalimbali, moja wapo ikiwa nikukosekana ushirikiano wakutosha  kwa  baadhi ya wateja ambao kwa makusudi wamekuwa wakifunga nyumba zao na kukimbia pindi wawaonapo wafanyakazi wa shirika hilo hasa wanapoandamana na askari polisi.
Katika hatua nyingine, Mgasa alisema kuna baadhi ya  maeneo ambayo wateja wanaotuhumiwa kufanya vitendo vya hujuma kwa kuiba umeme, shirika limepokea taarifa hizo ambapo limefika katika maeneo hayo na kusitisha huduma kwa wateja hao ikiwa ni pamoja kuwakatia nya kwenye nguzo kwa ajili ya hatua nyingine.

MATOKEO YA CHAGUZI ZA CCM-NEC

CHAGUZI ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimeendelea katika maeneo mbalimbali nchini ambapo sura mpya zimezidi kutikisa na kuwabwaga makada wa muda mrefu.

Tanga Mjini

Mbunge wa Tanga Mjini, Bw. Omari Nundu, ameanguka vibaya katika kinyang’anyiro cha kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), baada ya kupata kura 127 kati ya kura 1,183 zilizopigwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu.

Uchaguzi huo ulikuwa na mchuano mkali kati ya Bw. Nundu na aliyekuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Bw. Salim Kisauji aliyeibuka ushindi baada ya kupata kura 556.

Kushindwa vibaya kwa Bw. Nundu ambaye alikuwa Waziri wa Uchukuzi, kunamuweka njia panda katika medani ya siasa. Baadhi ya wana CCM mjini hapa walidai kushindwa kwa Bw. Nundu ni ishara mbaya kwake kuweza kutetea kiti chake cha ubunge kwa tiketi ya CCM kwani idadi ndogo ya kura alizopata ni ishara kuwa hana nafasi tena katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Akitangaza matokeo hayo jana alfajiri, Msimamizi wa uchaguzi huo Bw. Acheny Maulid, alimtangaza Bw. Kisauji kuwa mshindi wa nafasi ya ujumbe wa NEC. Alisema kura zilizopigwa zilikuwa 1,183 wakati nane ziliharibika na kura 1,175 zilikuwa halali. Katika uchaguzi huo Bi. Saumu Bendera alipata kura 458 na Bw. Salehe Masoud akipata 34.

Katika nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tanga, kiti hicho kilichukuliwa na Bw. Kassim Mbuguni aliyepata kura 662,  akifuatiwa na Bi. Mwanshamba Pashua (354) ambapo Bw. Samwel Kamote ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya mbalimbali nchini alipata kura 200 na Bw. Salim Mazrui akipata 98. Kura zilizopigwa zilikuwa 1,034 zilizoharibika 18, ambapo kura halali zilikuwa 1,016.

Akizungumza baada ya kuthibitishwa kuwa mjumbe wa NEC, Bw. Kisauji, aliahidi kuendeleza mshikamano ili kuongoza harakati za kukiimarisha chama hicho, “Nitaongeza kasi ya kuisimamia kikamilifu Serikali Wilaya ya Tanga ambapo siku za karibuni, kulikuwepo na udhaifu mkubwa uliochangia kuleta malalamiko dhidi ya Serikali,” alisema na kuwa, aliyekuwa mpinzani wake Bi. Bendera ataendelea kushirikiana nae kuhakisha wanasimamia wote utekelezaji wa ilani ya chama hicho na kuzikomboa kata tisa zilizoko upinzani kutoka CUF ili zirejeshwe CCM.

Hata hivyo, aliyekuwa Mwenyekiti wa muda katika uchaguzi huo Bw. Athuman Makalo, aliwataka wagombea wote waende mbele kuelezea mazingira ya uchaguzi huo.

Baadhi ya wagombea walioshindwa waliondoka ukumbini ambapo Bi. Mwanshamba Pashua, ambaye alishika nafasi ya pili katika nafasi ya Uenyekiti wa CCM Wilaya, ndiye aliyekwenda kuwashukuru wapiga kura.

Bunda

Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, Wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, wapo katika ushindani mkali kila mmoja akihaha kusaka kura kwa wajumbe.

Katika uchaguzi uliofanyika jana, mgombea wa nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha, Bw. John Kitang’osa, ambaye ni Katibu wa mbunge wa Bunda, Bw. Stephen Wassira, alibwagwa na kijana Bw. Mukwabe Sila.

Mgombea mwingine katika nafasi hiyo alikuwa Bw. Sarate Mimi ambaye ni mmoja kati ya Maofisa Wakaguzi wa Ndani katika Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Nafasi ya Katibu Uenezi Wilaya ilichukuliwa na Bw. Janes Sariro, ambaye aliwabwaga Bw. Kondoro Bega na Bw. Juma Sanga.

Bw. Christopher Sanya, Bw. Makongoro Nyerere na Bw. Enock Chambili, ambao wanagombea nafasi ya Uenyekiti Mkoa, waliomba kura kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilayani humo ambapo uchaguzi huo utafanyika Oktoba 13 mwaka huu.

Akiomba kura kwa wajumbe hao, Bw. Sanya alisema vigogo ndani ya CCM ndio wanaoendekeza makundi hivyo ni vyema wanachama waingize sura mpya ili kuleta umoja ndani ya chama hicho, “Wanaodai kumaliza makundi ndani ya CCM wanasema kwa mdomo tu, lakini haitoki moyoni kwa sababu wameshika madaraka hayo siku nyingi, dawa ya kumaliza makundi ni kuwachagua makada wasioegemea upande wowote,” alisema Bw. Sanya na kuongeza: “Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, utakuwa mgumu kwa chama chetu kama viongozi ambao watachaguliwa wataendeleza siasa za makundi.”

Naye Bw. Makongoro Nyerere, alidai mwaka 2007 aliipokea CCM iliyosambaratika mkoani humo iliyojaa siasa ya chuki na makundi ambapo kazi aliyoifanya ni kurejesha umoja katika chama hicho. Alisema viongozi wa kitaifa ndio wanaosambaza tofauti zao hadi kwenye matawi ya chama na kusambaratisha wanachama.

Bw. Chambili alidai yeye ni kiongozi asiyeogopa upinzani na yuko tayari kuhakikisha hakuna jimbo ambalo litachukuliwa na upinzani mkoani humo kama watamchagua katika nafasi hiyo.

Hata hivyo baadhi ya wajumbe na makada wa CCM, walidai wagombea wote wa nafasi, wamekiuka agizo la Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, “Hivi karibuni akiwa mjini Dodoma kwenye kikao cha NEC, baada ya kupitishwa majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali, Rais Kikwete aliwahadharisha wagombea wa nafasi zote kutowafuata wapiga kura ili kuomba huruma yao kabla ya siku ya uchaguzi,” walisema wajumbe hao.

Same
Mkuu wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Bw. Clement Kapufi, aliibuka na ushindi katika nafasi ya wajumbe watano ambao wataiwakilisha Wilaya hiyo katika Mkutano Mkuu Taifa.

Wengine walioshinda katika nafasi hiyo ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bw. Christopher Irira, Ummy Mkumbwa, Bi. Veronica Mmbaga na Zabihuna Irigo.

Katika uchaguzi huo, Mwenyekiti wa CCM wilayani humo Bw. Augustine Kessy, alitetea nafasi yake baada ya kupata kura 855 dhidi ya Bw. Yahya Mnzava (324) na Azza Nisaghurwe (153).

Bw. Ali Mmbaga alishinda katika nafasi ya ujumbe wa NEC wilayani humo baada ya kupata kura 832, wakati Bw. Joseph
Kateri (438), ambapo Bw. Joseph Mnzava, alipita bila kupingwa kwenye nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha.

Mwanga

Mwenyekiti wa CCM aliyemaliza muda wake Bw. Urban Masewa, alitetea nafasi hiyo baada ya kupata kura 527 ambapo mpinzani wake Bw. Suleiman Mruttu aliepata kura 252.

Wakili wa kujitegemea Bw. Joseph Tadayo, alishinda ujumbe wa NEC wilayani humo baada ya kuzoa kura 535 dhidi ya Bw. Kuria Msuya, (255) na Kanali mstaafu Saidi Msuya (18).

Bw. Suleiman Mfinanga, alimrithi Waziri Mkuu mstaafu, Bw. Cleopa Msuya katika nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha,
baada ya kupita bila kupingwa.

Rombo
Bw. Wilbard Ringia alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM wilayani humo kwa kura 398 wakati Bw. Rogatus Matoli (300), ambapo Bw. Evod Mmmanda, alishinda ujumbe wa NEC wilayani humo kwa kura 380, Bw. Calisti Shirima (311) na Bw. Sabas Asenga aliepata kura 15. 

---
Taarifa hii ni kwa mujibu wa Waandishi wa habari Raphael Okello, Heckton Chuwa na Benedict Kaguo wa gazeti la Majira