Friday 5 October 2012

TANZANIA YAPOKEA MSAADA WA BILIONI 352 KUTOKA KWA WAJERUMANI

Ujerumani imetoa jumla ya shilingi bilioni 352( euro milioni 176) kwa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika kipindi miaka mitatu ijayo.
Makubaliano ya msaada huo yamesaini jana jijini na Waziri wa Fedha Dr. William Mgimwa kwa upande wa Tanzania na Balozi wa Ujerumani nchini Kluas Peter Brandes.
Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo kwa niaba ya Tanzania Waziri wa Fedha dr. Mgimwa alisema kuwa fedha hizo zitasaidia shughuli mbali za maendeleo katika kipindi cha mwaka 2012/13- hadi 2014/15.
Alisema kuwa msaada huo unalenga maeneo ya kuboresha utawala bora katika serikali za mitaa, kusaidia sekta ya afya , nishati , maliasili, maji, na kuboresha programu ya usimamizi wa fedha za umma.
Dr. Mgimwa aliongeza kuwa eneo jingine ambapo hizo zitaelekezwa ni pamoja na kusaidia mfuko wa bajeti kwa kipindi miaka mitatu hiyo na kusaidia ofisi ya Taifa ya Mkaguzi wa hesabu za serikali .
Alisema kuwa miradi hiyo itasaidia kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) na hivyo kuboresha hali ya uchumi na kijamii ya wananchi.
Aidha Waziri huyo wa Fedha alimuhakikisha Balozi wa Ujerumani nchini kuwa , Serikali itahakikisha fedha za msaada zinatuma katika maeneo yalipangwa kwa manufaa ya wananchi ili matokeo yake yaweze kuonyesha thamani ya fedha waliyotoa.
Naye Balozi Brandes alisema kuwa Nchi yake itaendelea kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu na Tanzania ili kufikia malengo ya kupambana na umaskini na hivyo kuboresha maisha ya Watanzania hasa waishio vijijini.
Aliongeza kuwa msaada waliotoa utasaidia wakazi wa mijini kupata maji safi na salama kwa ajili ya kujikinga na magonjwa yatokanayo na maji yasiyo salama.

No comments: