CHAGUZI
ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimeendelea katika maeneo
mbalimbali nchini ambapo sura mpya zimezidi kutikisa na kuwabwaga makada
wa muda mrefu.
Tanga Mjini
Mbunge
wa Tanga Mjini, Bw. Omari Nundu, ameanguka vibaya katika kinyang’anyiro
cha kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), baada ya
kupata kura 127 kati ya kura 1,183 zilizopigwa na wajumbe wa Mkutano
Mkuu.
Uchaguzi huo ulikuwa na mchuano mkali kati ya Bw. Nundu na
aliyekuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Bw. Salim Kisauji aliyeibuka
ushindi baada ya kupata kura 556.
Kushindwa vibaya kwa Bw.
Nundu ambaye alikuwa Waziri wa Uchukuzi, kunamuweka njia panda katika
medani ya siasa. Baadhi ya wana CCM mjini hapa walidai kushindwa kwa Bw. Nundu ni ishara mbaya kwake kuweza kutetea kiti chake cha ubunge kwa tiketi ya CCM kwani idadi ndogo ya kura alizopata ni ishara kuwa hana nafasi tena katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Akitangaza
matokeo hayo jana alfajiri, Msimamizi wa uchaguzi huo Bw. Acheny
Maulid, alimtangaza Bw. Kisauji kuwa mshindi wa nafasi ya ujumbe wa
NEC. Alisema kura zilizopigwa zilikuwa 1,183 wakati nane ziliharibika na
kura 1,175 zilikuwa halali. Katika uchaguzi huo Bi. Saumu Bendera
alipata kura 458 na Bw. Salehe Masoud akipata 34.
Katika nafasi
ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tanga, kiti hicho kilichukuliwa na Bw.
Kassim Mbuguni aliyepata kura 662, akifuatiwa na Bi. Mwanshamba Pashua
(354) ambapo Bw. Samwel Kamote ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya
mbalimbali nchini alipata kura 200 na Bw. Salim Mazrui akipata 98. Kura
zilizopigwa zilikuwa 1,034 zilizoharibika 18, ambapo kura halali
zilikuwa 1,016.
Akizungumza baada ya kuthibitishwa kuwa
mjumbe wa NEC, Bw. Kisauji, aliahidi kuendeleza mshikamano ili kuongoza
harakati za kukiimarisha chama hicho, “Nitaongeza kasi ya kuisimamia
kikamilifu Serikali Wilaya ya Tanga ambapo siku za karibuni, kulikuwepo
na udhaifu mkubwa uliochangia kuleta malalamiko dhidi ya Serikali,”
alisema na kuwa, aliyekuwa mpinzani wake Bi. Bendera ataendelea
kushirikiana nae kuhakisha wanasimamia wote utekelezaji wa ilani ya
chama hicho na kuzikomboa kata tisa zilizoko upinzani kutoka CUF ili zirejeshwe CCM.
Hata
hivyo, aliyekuwa Mwenyekiti wa muda katika uchaguzi huo Bw. Athuman
Makalo, aliwataka wagombea wote waende mbele kuelezea mazingira ya
uchaguzi huo.
Baadhi ya wagombea walioshindwa waliondoka ukumbini
ambapo Bi. Mwanshamba Pashua, ambaye alishika nafasi ya pili katika
nafasi ya Uenyekiti wa CCM Wilaya, ndiye aliyekwenda kuwashukuru wapiga
kura.
Bunda
Wilaya
ya Bunda, mkoani Mara, Wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa,
wapo katika ushindani mkali kila mmoja akihaha kusaka kura kwa wajumbe.
Katika
uchaguzi uliofanyika jana, mgombea wa nafasi ya Katibu wa Uchumi na
Fedha, Bw. John Kitang’osa, ambaye ni Katibu wa mbunge wa Bunda, Bw.
Stephen Wassira, alibwagwa na kijana Bw. Mukwabe Sila.
Mgombea
mwingine katika nafasi hiyo alikuwa Bw. Sarate Mimi ambaye ni mmoja
kati ya Maofisa Wakaguzi wa Ndani katika Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Nafasi ya Katibu Uenezi Wilaya ilichukuliwa na Bw. Janes Sariro, ambaye aliwabwaga Bw. Kondoro Bega na Bw. Juma Sanga.
Bw. Christopher Sanya, Bw. Makongoro Nyerere na Bw. Enock Chambili, ambao wanagombea nafasi ya Uenyekiti Mkoa, waliomba kura kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilayani humo ambapo uchaguzi huo utafanyika Oktoba 13 mwaka huu.
Akiomba kura kwa wajumbe
hao, Bw. Sanya alisema vigogo ndani ya CCM ndio wanaoendekeza makundi
hivyo ni vyema wanachama waingize sura mpya ili kuleta umoja ndani ya
chama hicho, “Wanaodai kumaliza makundi ndani ya CCM wanasema kwa mdomo tu, lakini haitoki moyoni kwa sababu
wameshika madaraka hayo siku nyingi, dawa ya kumaliza makundi ni
kuwachagua makada wasioegemea upande wowote,” alisema Bw. Sanya na
kuongeza: “Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, utakuwa mgumu kwa chama chetu kama viongozi ambao watachaguliwa wataendeleza siasa za makundi.”
Naye
Bw. Makongoro Nyerere, alidai mwaka 2007 aliipokea CCM iliyosambaratika
mkoani humo iliyojaa siasa ya chuki na makundi ambapo kazi aliyoifanya
ni kurejesha umoja katika chama hicho. Alisema viongozi wa kitaifa ndio
wanaosambaza tofauti zao hadi kwenye matawi ya chama na kusambaratisha
wanachama.
Bw. Chambili alidai yeye ni kiongozi asiyeogopa
upinzani na yuko tayari kuhakikisha hakuna jimbo ambalo litachukuliwa na
upinzani mkoani humo kama watamchagua katika nafasi hiyo.
Hata hivyo baadhi ya wajumbe na makada wa CCM, walidai wagombea wote wa nafasi, wamekiuka agizo la Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, “Hivi karibuni akiwa mjini Dodoma kwenye kikao cha NEC, baada ya kupitishwa majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali, Rais Kikwete aliwahadharisha
wagombea wa nafasi zote kutowafuata wapiga kura ili kuomba huruma yao
kabla ya siku ya uchaguzi,” walisema wajumbe hao.
Same
Mkuu
wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Bw. Clement Kapufi, aliibuka na
ushindi katika nafasi ya wajumbe watano ambao wataiwakilisha Wilaya hiyo
katika Mkutano Mkuu Taifa.
Wengine walioshinda katika nafasi
hiyo ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bw. Christopher Irira,
Ummy Mkumbwa, Bi. Veronica Mmbaga na Zabihuna Irigo.
Katika
uchaguzi huo, Mwenyekiti wa CCM wilayani humo Bw. Augustine Kessy,
alitetea nafasi yake baada ya kupata kura 855 dhidi ya Bw. Yahya Mnzava
(324) na Azza Nisaghurwe (153).
Bw. Ali Mmbaga alishinda katika nafasi ya ujumbe wa NEC wilayani humo baada ya kupata kura 832, wakati Bw. Joseph
Kateri (438), ambapo Bw. Joseph Mnzava, alipita bila kupingwa kwenye nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha.
Mwanga
Mwenyekiti
wa CCM aliyemaliza muda wake Bw. Urban Masewa, alitetea nafasi hiyo
baada ya kupata kura 527 ambapo mpinzani wake Bw. Suleiman Mruttu
aliepata kura 252.
Wakili wa kujitegemea Bw. Joseph Tadayo,
alishinda ujumbe wa NEC wilayani humo baada ya kuzoa kura 535 dhidi ya
Bw. Kuria Msuya, (255) na Kanali mstaafu Saidi Msuya (18).
Bw. Suleiman Mfinanga, alimrithi Waziri Mkuu mstaafu, Bw. Cleopa Msuya katika nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha,
baada ya kupita bila kupingwa.
Rombo
Bw. Wilbard Ringia alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM wilayani humo kwa kura 398 wakati Bw. Rogatus Matoli (300), ambapo Bw. Evod Mmmanda, alishinda ujumbe wa NEC wilayani humo kwa kura 380, Bw. Calisti Shirima (311) na Bw. Sabas Asenga aliepata kura 15.
---
Taarifa hii ni kwa mujibu wa Waandishi wa habari Raphael Okello, Heckton Chuwa na Benedict Kaguo wa gazeti la Majira
No comments:
Post a Comment