Thursday 13 September 2012

WALIMU WAPINGA KAMATI ILIYOTEULIWA NA SERIKALI


Chama cha walimu Tanzani CWT kimeitaka serikali kuacha kuwadanganya kama watoto  kufuatia Serikali kuzindua Baraza la pili la majadiliano ya pamoja kwenye utumishi wa  walimu lililozinduliwa jana  na Naibu waziri wa Elimu na Mafunzo  ya Ufundi  Mhe, Nlugo  na kuhudhuriwa na  wawakilishi wa CWT. Ambapo CWT imesema kuwa Baraza hilo halina mamlaka ya kutatua migogoro  sehemu ya kazi au migogoro  iliyokwisha jitokeza baina ya Watumishi wa Serikali na Serikali.


Rais wa CWT Bw, Gratian Mukoba  amesema  leo wakati anaongea na waandishi wa Habari kuwa  Kazi ya Baraza hilo ni kuishauri serikali kuhusu njia mbalimbali za kuzuia kutokea kwa migogoro na hiyo ni kwa mujibu  wa kifungu cha Sita cha Sheria ya majadiliano  ya pamoja  kwenye utumishi wa umma ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake za mwaka 2005.


Amesema kuwa  Chombo pekee chenye uwezo wa kushughulikia migogoro ni Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ambapo chama kilipeleka mgogoro wake na kufikia hatua ya kutoelewa.
Ameishauri Serikali  kufungua upya jalada la majadiliano kwani chama kinaamini kuwa walimu wamerudi kazini wakiwa hawana ari ya kufanya kazi  kwani wanasubiri majadiliano kufanyika  kwa ajili ya mwaka ujao wa Fedha, hivyo ili kuwatia Moyo walimu  na kuwaongezea ari ya kufanya kazi  madai yao yanahitaji kusikilizwa ndani ya mwaka huu wa Fedha.

No comments: